Mbowe: Hakuna utaratibu wa kumsafirisha Lissu, amshangaa Waziri Ummy Mwalimu

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kwa sasa hakuna utaratibu wa kumsafirisha Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kwenda Marekani au Ujerumani kutokana na ushauri wa madaktari wanaomtibu.
Akizungumza leo Ijumaa jijini hapa, Mbowe amesema madaktari wamesema hawezi kwenda popote kutokana na hali yake.
Amesema baada ya awamu ya kwanza ya matibabu aliyoyapata katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7, ya pili inafanyika Nairobi, Kenya alipo sasa.
"Awamu ya tatu itaamua aende wapi ambayo itahusu mazoezi," amesema Mbowe.
Mbowe amemshangaa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kusema kuwa Serikali iko tayari kumtibu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu popote duniani.
Mbowe ametoa mshangao huo leo Ijumaa alipokuwa akitoa taarifa kuhusu matibabu ya Lissu yanayoendelea jijini Nairobi.
Amesema wakati walipoamua kumpeleka Lissu jijini Nairobi, Waziri Ummy alikuwepo lakini walitaka Lissu apelekwe Muhimbili.

No comments:

Post a Comment