Mahakama Kutoa Maamuzi Kesi ya Mbowe na Wenzake May 15

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatarajia May 15,2018 kutoa uamuzi wa kesi ya kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali inayowakabili viongozi 9 wa CHADEMA akiwemo Freeman Mbowe kama iende Mahakama Kuu ama laa.

Hatua hiyo inatokana na mvutano wa hoja za kisheria zilizotolewa jana na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kisha kujibiwa leo na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Katika majibu yake Wakili Nchimbi ameiomba mahakama hiyo kutupilia mbali hoja za utetezi zilizotolewa na Kibatala kwa sababu zitapelekea ucheleweshaji wa shauri hilo pasipokuwa na sababu za msingi.

Nchimbi amedai kuwa katika mazingira ya mwenendo wa kesi hiyo toka ilipoanza hadi leo hakuna swali lolote la msingi lililoibuliwa na upande wa utetezi ambalo linajikita na uvunjifu ama ukiukwaji wa haki ya kikatiba.

“Nasema hivyo kwa sababu ukiangalia msingi wa hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi jana zimejikita katika mashtaka yanayowakabili washtakiwa” -Nchimbi

No comments:

Post a Comment