Kenyatta: Makubaliano yangu na Ruto ni imara

Mwananchi
Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta Jumapili alikaribia kabisa kumuunga mkono hadharani Naibu wake William Ruto kuwania kiti hicho cha juu mwaka 2022, akituliza hofu kwamba hatua yake ya kushikana mkono na kiongozi wa ODM Raila Odinga hatimaye atamtosa rasmi makamu wake.
Katikati ya wakati mgumu aliojikuta nao mbele ya viongozi wa mitaa juu ya madai kwamba kushikana kwake mkono na Raila kulizua msuguano kati yake na naibu wake, Rais Kenyatta alivilaumu vyombo vya habari kwa taarifa hizo.

"Nilichowaambia mara ya mwisho hapa kiko vilevile: magazeti yataandika mambo mengi. Hebu zingatieni kile tunachofanya. Kitu muhimu ni maisha yenu. Waacheni waandike kile wanachotaka lakini sijali. Nitalala usingizi usiku, "alisema Rais.

Kenyatta alizungumza katika uwanja wa maonyesho wa Kapsabet huko Nandi ambako alisaidia kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kibiashara kwa ajili ya Kanisa la Anglikana.
Viongozi kutoka Bonde la Ufa waliozungumza walikuwa na shauku ya kutaka kusikia kama Rais ataunga mkono jitihada za Ruto kumrithi yeye atakapostaafu na kuondoka miaka minne ijayo.
"Bado tunaamini katika mpango wenu wa miaka 10. Wala hatuna haja ya kuhoji unachotuambia. Tutaunga mkono ajenda ya mambo Manne Makubwa na mara moja muhula wako utakapomalizia naibu wako atachukua nafasi yako. Bado tunaendelea kuamini makubaliano yenu ya mwaka 2012 kwamba yako imara," alisema Seneta wa Nandi Samson Cherargei, ambaye amekuwa sauti inayoongoza dhidi ya mkakati wa kumuweka kando Ruto katika serikali.

No comments:

Post a Comment