TTB YAFURAHISHWA NA KUREJEA KWA SAFARI ZA SHIRIKA LA NDEGE LA QATAR

Ndege ya shirika la Qatar punde baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es salaam.
Mgeni akipimwa joto la mwili punde aliposhuka kutoka katika ndege
Wageni wakisimama kwa kusingatia alama zinazowaongoza kusimama umbali wa mita moja zilizowekwa na uongozi wa JNIA
Mizigo yz wageni ikipuliziwa dawa kabla ya kuruhusiwa kuzunguka katika mashine ya kusambazia mizigo.
Wageni wakisubiri mizigo yao kwa kufuata utaratibu wa kusimama umbali wa mita moja.

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) inaendelea kufuatilia utekelezaji wa mwongozo wa uendeshaji shughuli za Utalii nchini Tanzania wakati huu wa janga la Corona kwa kushiriki katika mapokezi ya ndege ya shirika la Qatar Airways ilioanza tena safari za kuja nchini Tanzania baada ya kusitisha safari zake kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19.

Ndege hiyo iliyowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere ikiwa na abiria 119 mali ya Shirika la ndege la Qatar limerejesha safari zake za kuja nchini mara tatu kwa wiki kwa kuanzia.

Wakati wa mapokezi ya ndege hiyo, Meneja Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi Mindi Kasiga alisema ujio wa ndege hii ya Qatar kwa mara nyingine tena nchini kwetu, umeongeza kasi ya kutangaza utalii wa Tanzania. “Sasa tupo tayari kupokea watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani ambao wanaweza kusafiri na Shirika la ndege la Qatar” alisema Bi Kasiga.

Wakati wa mapokezi ya ndege hiyo, Bodi ya Utalii Tanzania iliongozana na waandishi wa habari ilipongeza uongozi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo Dar es Salaam kwa namna walivyozingatia muongozo uliotolewa na Wizara ya Afya kwa wasafiri kama njia ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19”.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa uwanja wa ndege terminal III, Mhandisi Komba alisema “kama mlivyojionea hapa uwanjani, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA) tumejipanga vizuri na tunazingatia miongozo ya afya ya kitaifa na kimataifa wakati wa janga hili la Corona. Tunaanza kupokea ndege za mashirika mbalimbali zinazoanza tena safari zao nchini Tanzania. Tumeweka vifaa mbalimbali vikiwemo; vipima joto, vitakasa mikono pamoja na kuzingatia umbali wa mita moja. Hii yote ni katika kuhakikisha tunawalinda watumishi na wasafiri watakaowasili kupitia uwanja wa JNIA” Mhandisi Komba alisisitiza.

Aidha, ujio wa ndege ya shirika la Qatar ni matokeo chanya ya hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania ikiwemo kufungua tena anga la Tanzania kuruhusu safari na shuguli nyingine za kibiashara kuendelea.

No comments:

Post a Comment