Kenya Yaruhusu Ndege Nchi 11, Tanzania Haimo

Kenya Yaruhusu Ndege Nchi 11, Tanzania Haimo

IKIWA siku kadhaa kabla ya kuanza kwa safari za ndege kimataifa, serikali ya Kenya imetangaza mwongozo mpya kuhusu hatua hiyo.

Akizungumza jijini Nairobi wakati akitoa taarifa kuhusu mwenendo wa maambukizi ya janga la Covid-19 nchini Kenya, Waziri wa Usafirishaji James Macharia amesema kuwa anga la Kenya halitafunguliwa kwa kila mtu. Orodha ikionyesha wazi Tanzania ikiwa si mmoja wa nchi inayokaribishwa kwenye anga ya Kenya.

Macharia amesema ni raia wa nchi 11 pekee wa kigeni ndiyo watakaoruhusiwa kutua Kenya katika viwanja vyake vinne vya kimataifa vilivyopo Nairobi, Mombasa, Eldoret na Kisumu. Nchi zilizoruhusiwa ni China, Korea Kusini, Japan, Canada, Zimbabwe, Ethiopia, Switzerland, Uganda, Rwanda, Namibia na Morocco.

Waziri huyo amesema nchi hizo zimedhibiti janga la Covid- 19 kwa kiasi cha kuridhidha. Amesema nchi hizo zimepunguza maambukizi ya ugonjwa huo na raia wake wamekuwa wakipata dalili za kawaida za ugonjwa wa mfumo wa upumuaji.

”Tutaendelea kuboresha orodha yetu kwa kutegemea hali ilivyo na mazingira. Hii ni orodha yetu kwa leo tutaipitia tena kesho na siku zinazokuja,” alisema.

”Abiria wote watakaowasili kwa ndege za kimataifa wakiwa na hati zinazoonyesha kuwa hawana dalili za Covid-19 na wale waliopima saa 96 kabla ya safari hawatakaa karantini,” alisema.

Mara tu orodha ilipotolewa, Wakenya kwa haraka waligundua kuwa Tanzania haimo. Siku ya Jumatatu tarehe 27 mwezi Julai, Rais Uhuru Kenyatta alitoa kauli ambayo haikuilenga Tanzania moja kwa moja kuwa Kenya haifichi idadi ya watu wenye maambukizi ya Covid-19.

”Sisi tuko wazi na tunajua fika kuwa ugonjwa huu upo, tofauti na majirani zetu ambao wanauficha ukweli huu,” alisema Kenyatta.


No comments:

Post a Comment