Heka heka jijini Dar wakati watu wakijilinda usalama wao na mali zao dhidi ya kundi la Panya Road. |
Na Baraka Mfunguo,
Panya
road walivamia jiji la Dar jana ikidaiwa chanzo chake ni mwanachama mwenzao
aliuawa na sungusungu walipokwenda kuiba. Walipitisha michango na mida ya saa
kumi jioni walikusanyika magomeni kagera karibu na Friends corner hotel kwa
ajili ya mazishi. Kundi kubwa kama la vijana miatano lililosemakana kuwa
wanasubiri kwenda kwenye mazishi lilikuwa kwenye mkumbo wa kundi Panya Road.
Inasemekana walipeana taarifa maeneo yote na viunga vyote vya jiji la Dar waje
kushirikiana ili wakimaliza kuzika waanze kulipa kisasi ingawa haijathibitika
kama dhima yao ilikuwa ni kulipiza kisasi ama kuzika ama ni matokeo ya kifo cha
mwenzao inayeelezwa aliuawa.
Ilipofika
muda wa kwenda kuzika inaelezwa walifunga barabara na kuanza kuwapora makonda
wa daladala na baadhi ya watu huku wakiwa wakielekea makaburi ya Kagera
Mikoroshini, kipindi hicho polisi walipata taarifa na wakapishana nao wao
wakidhani wanaenda kuzika katika makaburi ya Mburahati . Maiti ilizikwa kwa
amri na utaratibu wao huku mashekhe wakishurutishwa na mapanga kwa mujibu wa
vyanzo vya taarifa .
Walipotoka
kuzika ikawa wakarudi kupitia njia ya Morogoro road nakuanza uporaji hadi polisi
wa kutuliza ghasia walipofika na kuanza kupiga mabomu, na kufanikiwa kuwakamata
wawili.Baada ya kutawanyika, wale waliokuwa wanaoenda mbagala wakawa wanapora
watu ovyo ovyo ,waliokuwa wakielekea Buguruni Tabata na Gongolamboto vivyo hivyo
na kundi lililokuwa linadaiwa la Mwananyama ndilo lilirudi tena usiku na kuishia
kukabiliana na polisi wa kutuliza ghasia .
Vijana
hawa
wadogo kiumri ukiwatazama
umri wao unaweza ukakadiria ni kati ya kuanzia miaka
14-23 .
Matokeo
ya kuasisiwa kwa makundi kama haya ambapo Mtwara lipo kundi maarufu la “Tukale
Wapi” ni ni matokeo ya kukosa ajira, rushwa, kukosa elimu na pengo lililopo kati
ya walionacho na wasionacho, upendeleo serikalini, hali mbaya ya kiuchumi,
kukata tamaa ya maisha, pamoja na wanasiasa kukosa mbinu na ubunifu wa kutatua
matatizo yao badala yake wanageuzwa ngazi ya kupandia, ugoigoi wa viongozi na
watendaji wa serikali katika kufikiri, NGO's zinazowatumia kama mitaji ya kupata
vipato na kuvimbisha matumbo ya wamiliki wake ambao hupita na kujitapa mbele za
watu na vyombo vya habari kama wanaharakati. Vile vile Ufisadi na ukosefu wa
maadili kwa viongozi wa nchi pamoja na wale waliopewa dhamana.
Wakati
kundi moja likionekana likiwa linaumia, kundi lingine la walionacho
linalojumuisha wasomi, wafanyakazi wafanyabiashara, wanasiasa na watu wenye
kipato cha kati linaonesha kutojali uhalisia. Jiulize wewe binafsi ni mara
ngapi umekutana na watoto wa mitaani ukiwa barabarani hususan wale
wanaojitafutia riziki walau ya kufuta kioo ili wapate ugali na kuonyesha
kutowajali na kufikia hata hatua ya kuwatisha na kuwatolea maneno machafu
yasiyoelezeka ama kuandikika.
Ama
kuwahi kusikia maswahibu yao kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na
Wizara pamoja na vyombo vyenye mamlaka husika vipo pamoja na watendaji wake na
havionyeshi kujali na jibu utakalopewa endapo utataka kujua kwa nini hali ya
watoto mitaani inaongezeka kila kukicha ni, "serikali haijatenga fungu la fedha
katika bajeti ya wizara" . Na hata kama serikali ingetenga fungu maalum kwa
watoto wa mitaani lingewafikia? Thubutu!
Hayo
ndio majibu mepesi kwa tukio ambalo sasa linakua na litafikia mahali
litawashinda. Sisemi litatushinda kwa sababu sidhani hata mimi ni miongoni mwao.
Mimi najichukulia kama raia wa kawaida kabisa kutokana na dhana ya baadhi ya
watu wenye madaraka, mamlaka , ajira na kipato kujiona wao wanastahili kuliko
wengine. Ni hali halisi ya kibinadamu mmoja mmoja na ubinafsi wa ndani lakini
sio hali halisi
ya
uhalisia wa maisha ya binadamu kwa ujumla
Wakati
wa enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hali haikuwa hivyo kulikuwa na
mikakati na mipango dhidi ya watoto wa mitaani na wale watukutu, japokuwa hali
haikuwa nzuri kifedha na kiuchumi, lakini iliweza kudhibitiwa . Nakumbuka pia
miaka ya mwanzoni wa tisini nikiwa mwanafunzi wa sekondari ya Tambaza, pale
maeneo Upanga (sikumbuki vizuri mtaa) kama unaenda Zanaki sec ukitokea njia ya
DIT(Zamani Dar Tech) usawa wa kanisa la Mennonite kutokea mchepuko Morogoro
road mkabala na iliyokuwa shirika la bahati nasibu, kulikuwa hata na mahabusu
yao kulikuwa hata na mjumuisho wa watoto wa mtaani na watukutu walikuwa
marafiki wazuri kutokana na malezi yao na sie tulikuwa tukipita njia tulikuwa
walau tukiwatupia karanga na matunda sasa hivi naambiwa hata magerezani na
mahabusu watoto na watu wazima huchanganikana.
Kimsingi
watoto wa mitaani walikuwa hawaonekani na kila mwananchi alijivisha jukumu la
kuhakikisha maadili yanakuwepo katika jamii kuanzia ngazi ya chini.
Sasa
imefika wakati huria ambapo watu huweza kuzaana na kutelekeza watoto, wengine
kutupa watoto katika mfuko ya plastiki sitaki kusema ya Rambo, watoto kukosa
malezi na misingi ya maadili, Elimu kugeuzwa biashara badala ya huduma ya
msingi, na hata hizo haki zao zinazoelezwa katika Katiba ibayopendekezwa ni kama
porojo tu za wanasiasa. Hao watoto wa mitaani wakiwa wamefikia hatua ya utu
uzima yale manyanyaso, uonevu, dhuluma, vitendo vinavyoshusha utu wa mtu ambavyo
vinafanywa na hao hao waliomo miongoni mwa watu wanaojiita wasomi, wanasiasa,
wajasiriamali, wanaharakati na watu wa kundi la kati na huku serikali iliwa
imefumbia macho matukio hayo, hali Fulani ya kisaikolojia hujitokeza
inayowafanya wachukie kila kitu na kila mtu.
Wakikutana
na watu wakawahamasisha wajiunge na kundi fulani la uhalifu kwa ujira fulani ama
kupata ulinzi dhidi ya vitendo vyovyote visivyostahili kufanyika kwao
watakataa?Haya yote kwa mtazamo wangu, inatokana na watu kuchoka mfumo
dhulumati, mfumo wa kimafia and "that anger manifest itself into those actions
for them to be heard" hiyo ndiyo fimbo ya mnyonge.
Mimi
binafsi sitashangaa kama haya yakitokea kulikuwa na "Komando Yosso" miaka ya
tisini baadae likaja kufa. Ikitokea Wananchi wakaamua kuanzisha makundi ya
kukabiliana na uhalifu kuna mtu ambaye yuko katika ngazi ya juu serikalini
(ukiacha Said Mwema aliyeanzisha polisi jamii ambalo nalo uhalali wake
haueleweki mpaka sasa) ataweza kuwapa msukumo na hamasa katika jamii hii ya
leo iliyojaa unafiki na uzandiki?
Tumezoea
kuwalaumu Polisi pale matukio mabaya yanayoyowagusa wengi (si mtu mmoja
mmoja)yanapotokea Ninaamini kwa hali hii ya ubadhirifu na ukosefu wa
maadili wa viongozi na wale waliohodhi dhamana serikalini kwa njia zao za ghilba
na kejeli dhidi ya wananchi, walalahoi na wasionachi, itafika wakati hata hao
panya road wakaonekana mashujaa endapo wakitumika vizuri kuuondoa uozo huu wa
rushwa na ufisadi uliojaa na kuifunika nchi gubi gubi na serikali kulala
fofofo.
Pamoja
na kwamba njia walizotumia zinahatarisha usalama wa wananchi na mali zao, ni
wakati wa kuchunguza na kubaini chanzo cha matatizo na kukata mzizi na sio tawi
kama wengi wanavyotaka iwe. Kukata tawi kwa mfano ni kuwatafuta kuwakamata na
kuwaua, badala yake wawekwe kitako watu waangalie uwezekano wa kuwasaidia na
kuwatumia kwa maendeleo ya nchi.
No comments:
Post a Comment