Moto wa Lowassa sasa watikisa CCM. Nape aibuka, ataka asikaribishe makundi kumshawishi urais.

Kufuatia makundi mbalimbali yanayojitokeza kwenda nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kumshawishi kugombea urais, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hatua hiyo itamfanya akose sifa za kugombea nafasi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari waliopo katika msafara wa Katibu Mkuu wa CCM waliotaka ufafanuzi kuhusu hali hiyo, Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema matendo yanayoendelea kufanywa na Lowassa, ambaye ni Mbunge wa Monduli ni kampeni za wazi zinazokiuka katiba na kanuni za chama hicho.

“Hivyo kuendelea nazo kunaweza kumfanya akose sifa za kugombea nafasi ya urais. Na anachofanya Lowassa ni kuvunja kanuni na kiburi. Ni matendo ya wazi ya kampeni. Bila shaka anajua adhabu yake. Matendo hayo yanaweza kumpotezea sifa za kuwa mgombea kupitia CCM,” alisema Nape.
Pia alisema Lowassa ni miongoni mwa wana-CCM sita waliopewa adhabu na CCM mwaka mmoja na kwamba, mpaka sasa bado wapo kwenye kipindi cha uangalizi wakati vikao husika vikiendelea na tathmini dhidi yao.

No comments:

Post a Comment