KIGOGO WA WEMA KORTINI

Haruni Sanchawa Makongoro Oging’
Jamaa aliyewahi kudaiwa kuwa karibu na mwigizaji Wema Sepetu anayejulikana kwa jina la Clement Mwankayi Kiondo ‘CK’ au Kigogo wa Wema na mwenzake, Emmanuel Kagondela wamepandishwa kortini kwa mashitaka mawili ya kughushi hundi kisha kuchota fedha.
Clement Mwankayi Kiondo ‘CK’ akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Wawili hao walipandishwa kizimbani juzi (Alhamisi) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar.
Katika kosa la kwanza, CK alidaiwa kutenda kosa la kughushi hundi no 302002 yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 100 kutoka kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu huku akijua kuwa ni kosa kisheria.
Katika kosa la pili, CK ambaye aliwahi kudaiwa kumgombanisha Wema na Kajala Masanja kwa pamoja na Emmanuel, mnamo Machi 13, 2014 walikula njama za kuiba kiasi cha Sh. milioni 100 katika Benki ya NBC, Tawi la Ilala jijini Dar.
Kesi hiyo ambayo ilisikilizwa mbele ya Hakimu Huruma Shahid na Wakili wa Serikali, Aloyce Mbumito, ilidaiwa  mnamo Machi, 2014 kwa nyakati tofauti, jamaa hao walitumiwa kughushi hundi kwenye ofisi hiyo ya Waziri Mkuu.
Katika kujibu tuhuma hizo, washitakiwa wote kwa pamoja  walikana mashitaka na kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 23, mwaka huu.
Katika kesi hiyo watuhumiwa hao walipaswa kuwa na wadhamini wawili-wawili wanaotambulika na kiasi cha Sh. milioni 10 kila mmoja kwa ajili ya kupatiwa dhamana.

No comments:

Post a Comment