Ukimwi kuisha Dar ni vigumu

Dar es Salaam: Hali ni mbaya kama si tete! Kikosi maalum cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ cha Global Publishers kimebaini kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi katika Jiji la Dar ni vigumu kuisha kutokana na asilimia 75 ya watu wanaoingia gesti madhumuni yao ni kufanya ngono na si kulala kama wageni, Ijumaa Wikienda lina uchunguzi kamili.
Mbaya zaidi, asilimia 25 ya watu hao ndiyo hutumia kinga kwa ajili ya ngono salama huku asilimia 75 wakiwa hawana haja ya zana hiyo yenye kukinga maambukizi ya virusi kama wenza wao wanayo.
OFM ilifanya utafiti kwenye gesti mbalimbali za Dar ili kupata mizani sahihi ya matumizi ya kinga kwenye gesti na pia kufahamu wateja wakuu kwa siku husika. Hapa hawazungumziwi wanaopata maambukizi nje ya ngono zembe.
OFM ilibaini kuwa, wateja wakuu kwenye gesti hizo ni kada zote lakini hasa wenye umri wa kuanzia miaka 22 na kuendelea huku machangudoa nao wakiwa mstari wa mbele kwa kuingia gesti na wateja wao hivyo kuwa sehemu kubwa ya maambukizi ya ugonjwa huo kwa sababu wao huunganisha mtandao mkubwa kwa siku.
Miongoni mwa gesti zilizotembelewa na OFM ni zile zilizopo, Sinza, Kinondoni, Buguruni, Temeke, Mbagala, Ilala na maeneo ya Tabata.
Baadhi ya wahudumu waliweka wazi kwamba, wateja wakubwa wanaoingia kwenye gesti za Dar ni wenyeji ambao huingia kwa lengo la kufanya ngono na si kulala kwa maana ya wasafiri au wale waliopungukiwa na malazi majumbani mwao kutokana na sababu mbalimbali.
WASIKIE WAHUDUMU
“Ni kweli Ukimwi kuisha Dar ni vigumu sana. Kwanza wateja wengi wanaokuja hapa kila siku, lakini wengi zaidi siku za wikiendi ni wenyeji wa hapahapa Dar.
“Utakuta mtu anaandikisha anatoka Dar kwenda Dar. Wengi si wageni, wanaingia kwa lengo la kufanya ngono na kuondoka, wanaolala mpaka asubuhi ni wachache sana. Na utaratibu huu umeua ‘shot time’.
“Siku hizi mtu analipia chumba kana kwamba analala mpaka kesho yake, lakini ikifika saa nne usiku anatoka na mwanamke wake,” alisema mhudumu wa gesti moja iliyopo maeneo ya Mwananyamala, Kinondoni.
Mwingine ambaye anahudumu gesti iliyopo Buguruni alisema: “Kwa kweli sisi tunaofanya kazi gesti ndiyo tunashuhudia mengi. Wengine wanaingia humu ni wake na waume za watu. Mbaya zaidi sisi tunaweka zana katika kila chumba lakini utashangaa wakishatoka, ukienda unakutana na pakti zako za zana kama ulivyoziweka. Hii ina maana kwamba, hawakutumia.”
Naye mhudumu aliyejitambulisha kwa jina moja la Jumaa kutoka gesti moja iliyopo Sinza-Kijiweni, yeye alisema:
“Kwa siku tunapokea wateja wengi wa Dar kuliko mkoa. Halafu hapa kwa kawaida mapokezi tuna maboksi ya zana ili wateja wanaoingia kwa kufanya ngono iwe ngono salama. Pakti moja tunauza shilingi mia tano, miaka miwili iliyopita, maboksi matano yalikuwa yakiisha kwa siku saba, siku hizi hayaishi hata matatu wakati wingi wa wateja ni uleule.
“Baadhi ya wahudumu walisema kuwa, kinachoonekana kwa siku hizi watu wameanza kuuzoea ugonjwa huo hatari tofauti na miaka mitatu iliyopita. Lakini sababu za kuuzoea wanazijua wao wenyewe.”
Baada ya utafiti huo, gazeti hili lilimtafuta Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecki Sadiki na kumuuliza kuhusu mikakati iliyopo ya kutokomeza biashara ya kuuza miili.
“Kwanza hakuna sheria inayomlazimisha mtu kutumia kinga. Kama mtu anaingia gesti anatakiwa kujua mwenyewe kwamba anatakiwa kutumia kinga.
“Lakini iko haja ya kutoa elimu zaidi kwa jamii ili waone umuhimu wa matumizi ya kinga. Zamani, kulikuwa na taasisi ambazo zinapeleka kinga kwenye nyumba za kulala wageni, sijui ziliishia wapi!”

No comments:

Post a Comment