HALI hii hutokana na viungo vya uzalishaji wa vichocheo vya uimarishaji uzazi kwa mwanamke na mwanaume kutofanya kazi. Viungo au Glandi hizi ni korodani kwa mwanaume na ovari kwa mwanamke.
CHANZO CHA TATIZO
Tatizo hili linaweza kuwa linatokea tangu kuzaliwa au linatokea katika mfumo mzima wa mwili. Kwa tatizo la kuzaliwa nalo, korodani au vifuko vya mayai huwa havifanyi kazi ya kuzalisha vichocheo au homoni zinazohitajika ambapo kwa korodani huzalisha homoni za kiume na ovari huzalisha homoni za kike.
Vyanzo vya matatizo ni kama vile:-
-Matatizo katika mfumo wa kinga mwilini.
-Matatizo katika mfumo wa vinasaba.
-Matatizo ya Ini na Figo.
-Mionzi iwe ya X-ray au viwandani.
-Upasuaji wa kuondoa korodani zote mbili au ovari zote mbili.
Matatizo ya vinasaba yanayotokea kwa wanawake huitwa Turner Syndrome na kwa wanaume huitwa Klinifelter Syndrome.
Katika matatizo mengine ya Hypogonadism mfumo wa ubongo unaohusisha Pituitary na Hypothalamus ambazo hudhibiti utolewaji wa homoni mwilini huwa haufanyi kazi vizuri hivyo husababisha matatizo ya mfumo wa mwili na uzazi ambapo vyanzo vikuu vinaweza kuwa;-
-Endapo mama mjamzito wakati wa kujifungua akatokwa na damu nyingi sana na ikija kukata inakata moja kwa moja, yaani hapati tena siku zake na uwezo wa kuzaa unapotea.
-Matumizi holela ya dawa zenye Steroids, mfano krimu za kufanya ngozi hasa ya uso ing’ae.
-Matatizo haya pia yanaweza kuwa ya kurithi endapo kwenye ukoo wenu wapo watu wenye matatizo katika mfumo wa uzazi wa aina hii.
-Maambukizi, hasa virusi wa aina yoyote yanaweza kuathiri mfumo wa uzazi.
-Lishe duni hasa kwa watoto wanaokaribia balehe huweza kuwadumaza na aidha kutobalehe au kuchelewa kubalehe.
-Kuwa na madini mengi ya chuma mwilini, na hili linategemea na mazingira ya kuishi na vyakula au vinywaji hasa kwa mama mjamzito na watoto.
-Mionzi ya X-Ray ya mara kwa mara na mionzi ya viwandani.
-Kupungua uzito kwa kasi au kujipunguza uzito sana, kwa mwanamke anaweza kupoteza siku zake au asivunje ungo, hivyohivyo kwa mwanaume hudumaa viungo vyake vya uzazi.
-Upasuaji wa viungo vya uzazi kama tulivyozungumza hapo awali, kuumia korodani utotoni au hata katika umri wa ujana.
Matatizo haya husababisha mtu asikue aonekane bado mdogo hata kama umri unaenda. Mwanaume mwenye tatizo hili linaweza kwenda mbali zaidi na kupoteza uwezo wa kunusa harufu ya aina yoyote.
DALILI ZA TATIZO
Dalili kwa mtoto wa kike ambaye hajavunja ungo, utamwona bado ni mtoto yaani habadiliki yupo vilevile tangu alipokuwa na umri wa miaka kumi hadi anafikisha ishirini, matiti hayakui, urefu haongezeki. Kama tatizo likitokea baada ya kuvunja ungo huhisi joto muda wote hata kama kuna baridi, nywele sehemu za siri na makwapani hupuputika zenyewe, hupoteza hamu ya tendo la ndoa kabisa na haendelei tena kupata siku zake na kufunga hata zaidi ya mwaka.
Ukiwa na dalili hizo, muone daktari kwa ushauri zaidi.
No comments:
Post a Comment