Na Dustan Shekidele, RISASI Mchanganyiko
MOROGORO: Msanii maarufu wa filamu za Kibongo, Wastara Juma, mwishoni mwa wiki iliyopita aligeuka gumzo wakati wa harambee maalum ya kuchangia madawati kwa njia ya kuosha magari iliyofanyika mjini hapa, ambapo wateja wengi walikuwa wakimgombea awaoshee magari yao.
Harambee hiyo iliyofanyika kwenye kumbi za Samaki Sport na Nyumbani park, iliandaliwa na kundi la wanawake wanaojiita Best Friends Forever (BFF) ambao waliosha magari ya wateja kwa lengo la kukusanya fedha za madawati kuunga mkono harakati za Rais Dk. John Pombe Magufuli kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini.
Mwandishi wetu alimshuhudia Wastara akiwa bize kuosha gari la mheshimiwa diwani wa Kata ya Mafiga, Spear Komanya huku wateja wengine nao wakimsubiri amalize kisha aoshe yao, jambo lililomfanya muda wote aonekane kuwa bize.
“Leo tumeamua kuja hapa kwa sababu watu wengi wenye magari huja kustarehe hapa kwa hiyo wakati wenyewe wakistarehe sisi tunapiga kazi kuhakikisha tunapata fedha za kununulia madawati,” alisema Wastara.
Alipoulizwa kama hayo ni maandalizi ya kugombea tena ubunge mwaka 2020 baada ya kuanguka kwenye kura za maoni kwenye uchaguzi mkuu uliopita ambapo alikuwa akiwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia viti maalum, Wastara alisema:
“Siyo kweli, kwanza baada ya kushindwa ubunge mwaka jana sitarajii kugombea tena nafasi hiyo mwaka 2020. Kumbuka kufanya kazi hizi za jamii nimerithishwa na marehemu mume wangu, Sajuki (Juma Kilowoko), unajua enzi za uhai wake tulianzisha kituo cha watoto yatima kilichopo Kimamba, Kilosa na mpaka leo nakihudumia kwa hiyo wala sifanyi kwa sababu ya siasa.”
No comments:
Post a Comment